Kwa mujibu wa Shirika la Habari AhlulBayt (a.s) — ABNA — Baada ya tukio hilo la kusikitisha katika Bandari ya Shahid Rajaei Bandar Abbas lililosababisha idadi ya mashahidi na majeruhi miongoni mwa raia wa Iran, Hezbollah ya Lebanon imetoa taarifa rasmi kuonesha mshikamano na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Katika taarifa hiyo, Hezbollah imewasilisha salamu za rambirambi kwa Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi Ayatollah Ali Khamenei (Mwenyezi Mungu amhifadhi), Rais Dk. Masoud Pezeshkian, serikali na taifa la Iran pamoja na familia za mashahidi.
Hezbollah imesisitiza mshikamano wake wa kina na taifa la Iran linalojulikana kwa kusimama imara, na imetangaza kuwa itaendelea kusimama pamoja na Jamhuri ya Kiislamu na watu wapendwa wa Iran.
Katika taarifa hiyo pia imesomwa: "Tunamuomba Mwenyezi Mungu awape Mashahidi wa tukio hili rehema isiyo na mwisho, awaponeshe haraka majeruhi, na alilinde Taifa la Iran dhidi ya kila aina ya mabaya."
Hezbollah ya Lebanon pia imeeleza kuwa ina imani kamili na nguvu na azimio la watu wa Iran, na ikasisitiza: "Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kwa kutegemea imani yake na dhamira thabiti, itapita katika msiba huu na itaendelea kwa nguvu zaidi katika njia ya maendeleo, mapambano na kutetea malengo ya Ummah wa Kiislamu."
Your Comment